Waziri wa mambo ya nje wa Iran Mohammad Javad Zarif , leo ameitaja hatua ya rais wa Marekani Donald Trump ya kuzuia wageni kutoka nchi saba zenye idadi kubwa ya Waislamu kama zawadi kubwa kwa watu wenye misimamo mikali na wanaowaunga mkono.
Aidha, Kupitia ukurasa wake wa Twitter, Zarif ameandika kuwa hatua hiyo itawekwa kwenye rekodi za kihistoria,ambapo Ijumaa iliyopita, Rais Trump alisaini agizo la rais litakaloruhusu mabadiliko makubwa kwenye sera za wahamiaji nchini Marekani, ikiwa ni pamoja na kusitisha kuingia kwa wakimbizi na kuzuia Visa kwa wasafiri kutoka Iraq, Iran, Libya, Somalia, Sudan, Syria na Yemen.
Waziri huyo wa mambo ya nje wa Iran ametoa taarifa inayosema Iran nayo itawazuia wamarekani kuingia nchini mwake, lakini hawatahusisha wamarekani waliomo nchini humo kihalali.
Hata hivyo Iran imefikia hatua hiyo huku kukiwa na zaidi ya Wairan milioni moja wanoishi nchini Marekani, hatua hiyo ya Rais Trump inatarajia kuzusha vurugu miongoni mwa wanafunzi, wafanyabiashara na familia zinazotembeleana kati ya nchi hizo mbili