Kocha mkuu wa timu ya taifa ya Morocco Herve Renard amekisifia kikosi chake kwa kazi kubwa waliyoifanya katika fainali za Afrika za mwaka huu, licha ya kushindwa kusonga mbele kwenye hatua ya nusu fainali.
Renard ambaye aliipa ubingwa wa Afrika timu ya taifa ya Zambia mwaka 2012 na kisha Ivory Coast mwaka 2015, amesema kikosi chake kilifanya kazi kubwa ya kupambana katika kila mchezo, lakini bahati haikuwa yao walipokutana na Misri.
Amesema lengo lake lilikua ni kuvuka kwenye hatua ya makundi ya AFCON 2017, na hilo liliwezekana, na kutinga katika hatua ya robo fainali ilikua ni hatua nyingine kubwa kwake na kwa wadau wote wa soka nchini Morocco.
Hata hivyo kocha huyo kutoka nchini Ufaransa, ameahidi kuyafanyia kazi mapungufu aliyoyaona katika kikosi chake kabla ya kuanza hatakati za kusaka nafasi ya kucheza fainali za Afrika za mwaka 2019 ambazo zitafanyika nchini Cameroon.
Wakati huo huo Herve Renard amewapa ushauri wa bure Burkina Faso kwa kuwataka kuwa makini watakaposhuka dimbani kucheza dhidi ya Misri hapo kesho.
Renard amesema Burkina Faso wanapaswa kuwa wakakamavu wakati wote kutokana na wapinzani wao kuwa na mbinu tofauti tofauti ambazo kama hawatokua nazo makini watapoteza kirahisi.