Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Amos Makalla, ametoa siku 14 kwa Halmashauri zote za Mkoa wa Mbeya kuhakikisha zinawaondoa watu wote waliovamia maeneo ya hifadhi ya misitu ya mlima Mbeya.
Aidha amesema agizo hilo pia liendane na suala la kudhibiti shughuli zote za kibinadamu kando kando ya vyanzo vya maji kwa kufuata sheria ya inayowataka kufanya shughuli zao umbali wa mita 60.
Makalla ametoa agizo hilo katika kilele cha upandaji miti mkoani Mbeya katika eneo la chanzo cha maji cha mto Hanzya kata ya Itagano jijini Mbeya.
” lazima agizo hili litekelezwe mapema sanjali na kufanya tathmini ya hali ya uharibifu wa mazingira katika maeneo yote, ni kazi bure kuendelea kupanda miti wakati ile iliyopandwa mwaka uliopita imehalibiwa kwa kukosa matunzo au kuharibiwa kwa shughuli za kibinadam,”amesema Makala.
Aidha, Makalla ameitaka jamii kujenga utamaduni wa kupanda miti ya vivuli na matunda kwenye maeneo yao hususani katika maeneo ya vyanzo vya maji kwani ni muhimu kwa maisha ya kila siku.
Kwa upande wake Afisa Misitu wa Mkoa wa Mbeya Joseph Butuyuyu, amesema kuwa mpango wa kuhifadhi safu ya Mlima Mbeya umeanza kwa mafanikio makubwa hasa kutokana kuungwa mkono na Waziri mwenye dhamana ya Mazingira January Makamba, mara baada ya kutembelea safu ya Mlima huo.