Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Dar es Salaam, Dkt. Valentino Mokiwa amejibu tuhuma mbalimbali zikiwamo za wizi wa fedha zilizo elekezwa kwake, huku akisema kuwa ni uzushi wenye lengo la kumchafua ili aondolewe kwenye nafasi hiyo.
Dkt. Mokiwa amedai mgogoro huo umezushwa kutokana na hofu ya uchaguzi wa Askofu Mkuu mpya mwakani na uongozi wa kutojiamini wa Askofu Mkuu, Dkt. Jacob Chimeledya.
Amesema kuwa kiini cha mgogoro katika kanisa hilo ambao umesababisha Dkt. Chimeledya kumwandikia barua umetengenezwa na wakubwa kwa kuwatumia watumishi wawili waliofukuzwa utumishi katika dayosisi ambao waliandaa mashtaka ili aonekane kuwa hafai.
“Kila shtaka lililotengenezwa dhidi yangu linafurahisha, linasikitisha, linachekesha kwa sababu malengo yake ni kuondolewa Mokiwa,” amesema Askofu Mokiwa.
Aidha,amesema kuwa madai ya kuitoa Dayosisi ya Dar es Salaam katika udhamini wa Kanisa la Anglikana Tanzania. Shtaka hilo linatokana na hoja ya dayosisi kutaka kutumia viwanja vyake katika uwekezaji na kwamba kiwepo kifungu cha kuwa na majadiliano katika uwekezaji huo.
Hata hivyo, Kuhusu ufujaji wa mali na kuingia mikataba mibovu, amesema havipo kama ni mikataba iliamuliwa na sinodi na kamati ya dayosisi na kwamba chombo hicho kina uwezo wa kurekebisha kama kuna makosa na tayari kimetengeneza kamati ya kupitia mikataba hiyo.