Kocha mkuu wa timu ya taifa ya Cameroon Hugo Broos anaamini hatua ya wachezaji wake kulipwa poshi zao kabla ya mchezo wa nusu fainali dhidi ya Ghana, itaongeza chachu ya kujituma ipasavyo.
Broos amefichua siri hiyo alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu mchezo wa hii leo, ambapo Cameroon watakua wakisaka heshima ya kutinga katika hatua ya fainali ya michuano ya Afrika na ikiwezekana kutwaa ubingwa wa kwa mara ya tano.
Amesema wachezaji wake wameonyesha furaha kubwa wakiwa kambini baada ya tukio hilo kujitokeza, na anaamini viongozi wa shirikisho la soka nchini Cameroon wamelipa posho hizo wakati muafaka.
Amesema wakati wa michezo ya hatua ya makundi na robo fainali, kwa asilimia kubwa wachezjai wake hawakua na furaha, japo walionyesha kupambana na kufikia wapo sasa.
Mwaka 2011 wachezaji wa timu ya taifa ya Cameroon waliwahi kugoma kucheza mchezo wa kimataifa wa kirafiki, kwa kushinikiza walipwe posho zao.
Pia waliwahi kufanya kitendo kama hicho kabla ya kuanza kwa fainali za kombe la dunia za mwaka 2014, jambo ambalo lilisababisha wachelewe kuwasili nchini Brazil zilipokua zikifanyika fainali hizo.
Kulipwa posho kwa wachezaji kabla ya mchezo wao wa leo dhidi ya Ghana, kumehisiwa huenda ilikua hofu kwa viongozi wa shirikisho la soka nchini Cameroon ambao huenda wangeaibika endapo wachezaji wangegoma.