Nchi za Afrika Mashariki zimekubaliana kuwa Makao Makuu ya Lugha ya Kiswahili kuwa Tanzania ambayo yatakuwepo Zanzibar.
Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Nape Nnauye, Bungeni Mjini Dodoma alipokuwa akitoa ufafanuzi juu ya jitihada mbalimbali ambazo Tanzania inazichukua katika kukuza Lugha ya Kiswahili katika ngazi ya Kimataifa.
Nape amesema kuwa maamuzi hayo ya kuifanya Tanzania kuwa Makao Makuu ya Lugha ya Kiswahili yametokana na Tanzania kuzalisha walimu wengi wa Kiswahili ambao wanatumika katika ngazi mbalimbali za elimu ndani na nje ya nchi.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Anastazia Wambura amesema kuwa Wizara hiyo kwa sasa inachukua hatua mbalimbali kuhakikisha kuwa vyombo vya habari vinakuwa mawakala wa kulinda Lugha ya Kiswahili.
Aidha, amesema kuwa Waandishi wa Habari wanajukumu kubwa la kuhakikisha Lugha hiyo inaendelezwa ipasavyo ikiwa ni pamoja na kuzingatia matumizi sahihi ya Lugha hiyo katika majukumu yao ya kila siku.
“Kutumia zana kama vile Kamusi na vitabu vya miongozo ya uandishi pamoja na kuhudhuria makongamano ya Kitaifa na Kimataifa ya Lugha ya Kiswahili inasaidia kuongeza ujuzi na weledi wa Lugha ya Kiswahili,”amesema Wambura.
Hata hivyo Wizara hiyo iko katika maandalizi ya Sera ya Lugha ambayo itabainisha majukumu ya Vyombo vya Habari katika matumizi na uendelezaji wa Lugha ya Kiswahili.