Rais wa Marekani, Donald Trump, amemteua Rex Tillerson, kuwa waziri wa mambo ya nje. Lakini bado anakabiliwa na upinzani mkali, ikiwamo pendekezo lake la Jaji wa Mahakama Kuu ya Marekani
Donald Trump amesema ikilazimika wanachama wa republican wachukue hatua ya kubadilisha sheria za Baraza la Seneti ili uteuzi wake wa, Neil Gorsuch, kama jaji wa mahakama Kuu uweze kuidhinishwa kwa wingi mdogo wa kura, badala ya kura 60 zinazohitajika kwa sasa ndani ya baraza hilo lenye wajumbe 100.
Wakati wa kampeni zake za urais, Trump aliahidi kuteua Jaji wa Mahakama Kuu anayepinga utoaji mimba na atakaefanya kazi ya kubadilisha sheria iliyohalalisha utoaji mimba nchini Marekani.
Aidha, wanaharakati mbalimbali wa kutetea haki za wanaotaka kutoa mimba wamelikosoa pendekezo hilo la Trump, nakusema Gorsuch ni tishio dhidi ya haki za uzazi za wanawake, pamoja na uamuzi wa kihistoria uliofanywa na Mahakama Kuu mwaka 1973 wa kuhalalisha utoaji mimba nchini Marekani.