Makali ya Wabunge wa Bunge la 11 dhidi ya ufisadi yalijidhihirisha mjini Dodoma jana baada ya kamati yao inayoshughulikia Katiba na Sheria kueleza ilivyoingiwa na hofu ya kuwapo harufu ya vitendo hivyo katika mradi wa ukarabati wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu.
Katika taarifa yake iliyowasilishwa bungeni mjini Dodoma, kamati imedai kubaini kuwa ukarabati huo kwenye Ofisi ya Makamu wa Rais iliyopo Mtaa wa Luthuli jijini Dar es salaam, umefanyika chini ya kiwango na hivyo imeagiza uchunguzi ufanyike ili kujiridhisha na matumizi ya fedha zilizotumika kwa kazi hiyo.
Akisoma taarifa bungeni, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mohamed Mchengerwa, amesema kuwa katika fungu la 31 la ofisi hiyo, kwenye mradi namba 6389 ambao kamati ilifanya ziara zake imebaini kuwa jengo hilo limejengwa chini ya kiwango.
Amesema kamati imebaini kuwa kulikuwa na matumizi yasiyoridhisha ya fedha za umma katika baadhi ya miradi na kuagiza mamlaka zinazohusika kufanya uchunguzi maalumu kuhusu matumizi ya fedha na ubora wa miradi hiyo na kutoa taarifa kwa kamati.
Mchengerwa amesema katika mradi huo, wameagiza ufanyike uchunguzi na hatua kali zichukuliwe kwa watendaji wote waliohusika.
Tangu Serikali ya awamu ya tano iingie madarakani Novemba, 2015, chini ya utawala wa Rais John Magufuli na makamu wake Samia Suluhu, kasi ya vita dhidi ya vitendo vya rushwa na ufisadi imeongezeka huku ikielezwa kuwa hakuna atakayesalimika pindi ikibainika kuwa anashiriki vitendo vya aina hiyo vinavyokwamisha ufanisi wa miradi mingi ya maendeleo.

Serikali kufanya uchunguzi wa changamoto mradi wa TASAF
Mnyika Ang'aka kuhusu malipo ya wananchi Mloganzila