Klabu ya Inter Milan imepata pigo la pili, baada ya kupoteza mchezo wa ligi ya nchini Italia mwishoni mwa juma lililopita dhidi ya mabingwa watetezi Juventus FC, waliochomoza na ushindi wa bao moja kwa sifuri.

Juventus walipata furaha ya ushindi kupitia kwa kiungo mshambuliaji wao kutoka nchini Colombia Juan Cuadrado, aliyefunga bao pakee na la ushindi katika mpambano huo uliounguruma mjini Turin.

Inter Milan walimaliza mchezo huo wakiwa pungufu baada ya kiungo mshambuliaji kutoka nchini Croatia Ivan Perisic kuonyeshwa kadi nyekundu na mwamuzi, katika dakika za lala salama.

Kiungo huyo alikumbana na adhabu hiyo baada ya kujaribu kupinga maamuzi ya mwamuzi. 

Na dakika chache zilizofuata nahodha na mshambuliaji wa Inter Milan Mauro Icardi alimpiga na mpira mwamuzi, tukio ambalo lilizua hisia tofauti kwa kudhaniwa huenda lilikua la makusudi ama la bahati mbaya.

Kufuatia matukio hayo mawili, kamati ya nidhamu ya shirikisho la soka nchini Italia (FIGC) imetangaza kuwafungia wachezaji hao kucheza michezo miwili ijayo, ambayo itakua dhidi ya Empoli pamoja na Bologna.

Hata hivyo Inter Milan wana nafasi ya kukata rufaa kupinga adhabu hizo kwa wachezaji hao, endapo wataona kuna mashiko ya kufanya hivyo.

Video: Kampuni ya DataVision kukomesha wizi wa mitandao katika mabenki
Andre Marriner Kuamua Man Utd Vs Southampton