Bosi wa vinara wa ligi ya nchini England Chelsea (Antonio Conte), alikuwa mmoja wa mashuhuda wa mpambano wa ligi ya nchini Italia, ambao ulimalizika kwa mabingwa watetezi Juventus FC wakichomoza na ushindi wa bao moja kwa sifuri dhidi ya Inter Milan.

Conte aliripotiwa kurejea uwanjani hapo kwa mara ya kwanza tangu alipoondoka nchini Italia mwanzoni mwa msimu huu, kwa ajili ya kumshuhudia kiungo mshambuliaji Juan Cuadrado, ambaye anaitumikia Juventus FC kwa mkopo akitokea Chelsea.

Cuadrado, ndiye alifunga bao la ushindi la Juventus FC katika mchezo huo ilipofika dakika ya 45.

Hata hivyo taarifa nyingine zinadai kuwa, meneja huyo aliyeipa ubingwa Juventus FC mara tatu mfululizo (2011–12, 2012–13 na 2013–14 ), alifika uwanjani hapo kwa ajili ya kumfuatilia mshambuliaji Paulo Dybala.

Tetesi za kumfuatilia Dybala zilichukua nafasi yake, baada ya Conte kuamua kuondoka uwanjani hapo katika dakika ya 83, kufuatia mshambuliaji huyo kutolewa nje na bosi wake Max Allegri.

Klabu ya Chelsea imekua sehemu ya klabu zinazotajwa kumuwania mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 23, lakini Conte hajawahi kumzungumzia mbele ya vyombo vya habari.

Real Madrid Kumpotezea Thibaut Courtois
Aubameyang Kumkimbiza Aguero Etihad Stadium