Kocha kutoka nchini Israel Avram Grant ameamua kuachana na kikosi cha Ghana, kwa kuamini ni wakati muafaka kwake kuondoka katika taifa hilo la Afrika ya magharibi, ambalo lilishiriki fainali za Afrika zilizomalizika nchini Gabon mwishoni mwa juma lililopita.
Mkataba wa Grant, ulikua unafikia kikomo mara baada ya fainali za AFCON 2017, lakini bado alikua na nafasi kubwa ya kukaa chini na viongozi wa chama cha soka nchini Ghana (GFA) ili kuangalia uwezekano wa kuendelea kufanya kazi kwa makubaliano mapya.
Grant amesema tayari ameshakutana na rais wa chama cha soka nchini Ghana (GFA) Kwesi Nyantakyi na kumfahamisha kuhusu maamuzi yake ya kutosaini mkataba mpya, hatua ambayo anaamini itamsaidia kusaka mahala pengine pa kufanya kazi yake kwa changamoto mpya.
Kocha huyo kwa mara ya kwanza alikiongoza kikosi cha Ghana katika fainali za Afrika za mwaka 2015, na alikifikisha katika hatua ya fainali kabla ya kufungwa na Ivory Coast kwa changamoto ya mikwaju ya penati.
Kwa mwaka huu Grant ambaye aliwahi kukinoa kikosi cha Chelsea kwa muda, alikishuhudia kikosi cha Black Stars kikimaliza kwenye nafasi ya nne baada ya kufungwa na Burkina Faso bao moja kwa sifuri na kabla ya hapo kilishindwa kufurukuta kwa Cameroon kwenye mchezo wa nusu fainali kwa kukubali kichapo cha mabao mawili kwa sifuri.
Ghana ina ukame wa kutwaa taji la Afrika kwa zaidi ya miaka 30, na iliaminiwa huenda mwaka huu wangefanikisha furaha iliyowaponyoka tangu mwaka 1982, lakini kwa bahati mbaya mambo yalikua magumu kwao.
Hata hivyo bado haijafahamika ni wapi Grant atakapoelekea kufanya kazi yake mpya, lakini kuna tetesi huenda akatimkia katika moja ya mataifa ya bara la Afrika.