Beki wa klabu ya West Bromwich Albion Allan Nyom amesema hajutii kutokua sehemu ya kikosi cha mabingwa wa bara la Afrika timu ya taifa ya Cameroon, ambacho kilitwaa ubingwa huo mwishoni mwa juma lililopita, kwa kuifunga Misri mabao mawili kwa moja.
Nyom ni miongoni mwa wachezaji waliogoma kuitikia wito wa kocha Hugo Broos kwa ajili ya fainali za Afrika za mwaka huu, lakini baadae alibadili mawazo na kutaka kujiunga na kikosi cha Simba wasioshindika, ila kocha huyo kutoka nchini Ublegiji alimkatalia kwa kumwambia milango ilikua imeshafungwa.
Beki huyo mwenye umri wa miaka 28, amesema ni hatua nzuri kwa taifa lake kutwaa ubingwa wa Afrika na imedhihirisha wachezaji waliokuwepo kikosini, walikua na malengo makubwa ya kuitetea nchi yao.
Hata hivyo Nyom amedai kwamba, hakua na nia mbaya ya kukataa wito wa kocha Broos, na ndio maana siku kadhaa baadae alikubali kujiunga na wachezaji wenzake, lakini katazo la kocha huyo lilimrudisha nyuma na kuendelea na shughuli zake za kuitumikia klabu ya Wet Brom.
Amesisitiza kuendelea kumuheshimu kocha huyo na kuheshimu maamuzi yake, na daima ataendelea kuwa raia wa Cameroon, na kama kutakua na uwezekano wa kuitwa kikosini amesema yupo tayari kuitikia wito.
Wachezaji wengine waliokataa kuitikia wito wa kocha Hugo Broos kwa ajili ya fainali za Afrika za mwaka huu ni Joel Matip – Liverpool, André Onana – Ajax Amsterdam, Guy Roland Ndy Assembe – Nancy, André Zambo Anguissa – Olympique Marseille, Ibrahim Amadou – Lille, Maxime Poundje – Bordeaux na Eric Choupo-Moting – Schalke 04.