Majibu ya vipimo vya MRI ya beki wa pembeni wa klabu ya Arsenal Hector Bellerin yametoka na kuondoa hofu kwa mchezaji huyo kukaa nje ya uwanja kwa kipindi kirefu.
Bellerin alishindwa kuendelea na mchezo wa mwishoni mwa juma lililopita dhidi ya Chelsea, baada ya kugongwa na Marcos Alonso, hali ambayo ilizua hofu kwa wachezaji, benchi la ufundi na mashabiki wa Arsenal.
Majibu ya vipimo vya MRI alivyofanyiwa beki huyo wa pembeni kutoka nchini Hispania, yameonyesha hana tatizo kubwa na tayari ameshapewa ruhusa ya kujumuika na wachezaji wenzake kwa ajili ya kujiandaa na mchezo wa mwishoni mwa juma hili dhidi ya Hull City.
Mapema hii leo beki huyo mwenye umri wa miaka 21, alitarajiwa kuwa sehemu ya wachezaji ambao wanaendelea na maandalizi ya kujiwinda na mchezo dhidi ya Hull City ambao utapigwa katika uwanja wa Emirates.
Jana klabu ya Arsenal ilionyesha kuwa na wasiwasi wa kukosa huduma ya mchezaji huyo, na ilitoa tahadhari kwa mashabiki wote duniani kwa kusisitiza huenda Bellerin, akakaa nje kwa kipindi kirefu.