Aliyekua nahodha na kiungo wa timu ya taifa ya Ujerumani Michael Ballack amemtaka kiungo wa Arsenal Mesut Ozil kuihama klabu hiyo endapo anahitaji mafanikio ya kutwaa mataji.

Ballack ambaye pia aliwahi kuwatumikia mabingwa wa soka nchini Ujerumani FC Bayern Munich, amesema Ozil amekua na wakati mgumu wa kuutendea haki uwezo wake wa kucheza soka tangu alipojiunga na The Gunners miaka minne iliyopita.

Amesema kuna haja kwa kiungo huyo kurejea nyumbani kwao Ujerumani na ikiwezekana ajiunge na FC Bayern Munich ambayo ina bahati ya kutwaa mataji karibu kila msimu.

Ballack ametoa ushauri huo kwa Ozil, huku mkataba wa Arsenal na mchezaji huyo ukisaliwa na muda wa miezi 18 kufikia kikomo, na kuna dalili za kiungo huyo kutosaini mkataba mpya.

Ballack aliuambia mtandao wa Sport Bild “Mesut ni mchezaji wa kipekee na ana uwezo mkubwa wa kucheza soka. Naamini analijua hilo kutokana na juhudi zake ambazo wakati mwingine zimekua chachu ya kuleta mafanikio ya kusaidia sehemu ya mambo yanapokua magumu ndani ya Arsenal.

“Kutokana na hali hiyo naamini klabu nyingi duniani zinatamani kuwa na mchezaji kama Ozil. “Lakini kama anahitaji kutwaa mataji, anapaswa kujiunga na klabu kubwa kama Bayern Munich.

“Ukiangalia mwenendo wa soka la nchi za England na China, ni vigumu kwa mchezaji kupata mafanikio ya kutwaa mataji kwa haraka, lakini kwa hapa Ujerumani hususan klabu kama Bayern Munich, suala hilo linawezekana.

Ozil aliwahi kucheza soka nchini kwao Ujerumani akiwa na klabu za Schalke 04 na Werder Bremen kabla ya kutimkia Hispania kujiunga na Real Madrid, ambapo alitwaa ubingwa wa ligi (La Liga) na kombe la Mfalme (Copa del Rey).

FC Barcelona Wapinga Kadi Ya Suarez, Busquets
Mwijage: Viwanda vitajengwa na sekta binafsi