Waziri wa Viwanda Biashara na Uwekezaji Charles Mwijage amesema kuwa viwanda vitajengwa na Sekta Binafsi, na kazi ya Serikali ni kutengeneza mazingira mazuri ya kujenga Viwanda hivyo.
Mwijage ameyasema hayo Bungeni, Mjini Dodoma alipokuwa akitoa majibu kuhusu ufinyu wa bajeti wa Wizara hiyo ikiwa itatosheleza kujenga Viwanda nchini, wakati wa uwasilishaji wa taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira.
Mwijage amesema kuwa, kazi kubwa inayofanywa na Serikali kufikia uchumi wa Viwanda ni kutengeneza mazingira mazuri ya kujenga viwanda ikiwa ni pamoja na kuwatafuta wawekezaji ambapo mpaka sasa Serikali imeshaongea na wawekezaji toka China, Uturuki na Misri na wote wameonyesha nia ya kujenga viwanda nchini.
Kwa upande wake Mbunge wa Chalinze Ridhiwani Kikwete amesema kuwa ni jukumu la kila kiongozi kushiriki katika ujenzi wa Viwanda kwa kutambua fursa zilizopo eneo ambalo analisimamia.
“Sera ya kuwa na Tanzania yenye Viwanda haitawezekana kwa kuiachia Wizara ya Viwanda peke yake bali kwa sisi wabunge pia kushiriki kupitia fursa ambazo zinatuzunguka,” amesema Ridhiwani.
Vilevile amesema kuwa ni muhimu Serikali kuendelea kuboresha hali ya umeme kwani Viwanda kwa asilimia kubwa vinaendeshwa kwa kutumia umeme wa kutosha na wa uhakika.
Nae, Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango amesema kuwa fedha zinazopelekwa Wizara ya Viwanda si kwa ajili ya kujenga viwanda bali kwa ajili ya kuzielekeza sekta binafsi zilipo fursa za kujenga viwanda.
Aidha, Mwijage amesema kwamba mpaka sasa jumla ya viwanda 2169 vimesajiliwa ambapo viwanda 170 vimesajiliwa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), viwanda 180 vimesajiliwa na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni, viwanda 1,843 vimesajiliwa na Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogo (SIDO) na viwanda 7 vimesajiliwa na Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) vikiwemo viwanda 3 vya madawa.