Kitendo cha Jeshi la Polisi kutaka kumkamata Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe, juzi baada ya kutoka bungeni, kilimfanya mbunge huyo kuondoka bungeni usiku wa manane kuamkia jana kwa msaada wa Spika wa Bunge, Job Ndugai.
Juzi, wakati Zitto akiwasilisha hoja bungeni kuhusu utaratibu wa wabunge, hasa wa upinzani kukamatwa na polisi bila utaratibu, alibainisha kuwa hata yeye amepewa taarifa kuwa akitoka nje ya viwanja vya Bunge atakamatwa,na kuahidi kulala bungeni ili kuwakwepa polisi.
Aidha, Baada ya wabunge wa upinzani kususia kikao cha Bunge juzi kutokana na hoja hiyo kupingwa na Naibu Spika, Dkt. Tulia Ackson, Zitto aliendelea kuwepo ndani ya eneo la Bunge hadi jana saa 6:25 usiku alipoondoka kwa msaada wa Ndugai aliyempatia usafiri.
Hata hivyo, kususia kikao kwa wabunge hao wa upinzani sambamba na Zitto kusakwa na polisi, jana asubuhi kulimfanya Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge kutaka Serikali na Bunge kufanya kazi kwa pamoja, huku akisema taarifa ya kukamatwa hovyo kwa wabunge ataifikisha kwa Ndugai aliyedai kuwa ataitolea tamko rasmi leo.
“Niliondoka saa 6 usiku ikiwa ni baada ya mashauriano kati yangu na Katibu wa Bunge Dkt. Thomas Kashilillah na Spika Ndugai ambaye aliwasiliana na IGP Ernest Mangu,” amesema Zitto.
Hata hivyo, baada ya majadiliano ya muda mrefu, IGP aliwasiliana na Kamanda wa Polisi mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa ambaye alibainisha kuwa mbunge huyo alikuwa akitafutwa kwa kutoa kauli uchochezi alipokuwa mkoani Shinyanga.