Mabingwa wa soka duniani, klabu ya Real Madrid wameanza harakati za kumuwania mshambuliaji wa Torino ya Italia Andrea Belotti.
Gazzetta dello Sport limeripoti kuwa, mtendaji mkuu wa klabu ya Torino Urbano Cairo, anatarajiwa kusafiri hadi mjini Madrid juma lijalo, kwa kufanya mazungumzo ya uhamisho wa mshambuliaji huyo, ambaye pia anatajwa kuwaniwa na klabu za Arsenal, Chelsea, Liverpool zote za England na AC Milan ya Italia.
Cairo anatarajiwa kufanya kikao na rais wa Real Madrid Florentino Perez, ambaye amejipanga kufanya maboresho kwenye kikosi cha The Merengues kufuatia maagizo ya meneja Zinedine Zidane .
Tetesi za awali zinadai kuwa, Perez ametenga kiasi cha Pauni milioni 84, kwa ajili ya uhamisho wa mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 23.
Usajili wa Belotti kama utakamilishwa klabuni hapo, kutakua na uwezekano mkubwa wa kuuzwa kwa mshambuliaji kutoka nchini Ufaransa Karim Benzema ambaye hatokua na nafasi ya kucheza kwenye kikosi cha kwanza.
Belotti tayari ameshaifungia Torino mabao 15 katika michezo 20 ligi ya Italia (Serie A) aliyocheza kwa msimu huu.