Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba, amesema kuwa vitu mbalimbali vinavyohusu Wizara yake na maswali anayokutana nayo kuhusu sakata la dawa za kulevya, tayari ameshapanga mikakati ya kuwakamata wahusika wote baada ya kufanya ziara katika baadhi ya mikoa.
Amesema kuwa vita ya madawa ya kulevya haijaanza leo,na hili linaloongelewa ni vita ya kila mtanzania ambapo ni lazima kushikamana ili kuweza kutokomeza tatizo hilo, aidha amesema kuwa tangu aingie kwenye wizara hiyo alikuta Kitwanga teyari alishakamata mapapa wakubwa wa biashara hiyo.
“Jambo moja tu ambalo nawahakikishia na ambalo nawaomba wote tuwe nalo, tusibadili lengo na kuna watu wengine walikuwa wanasema mbona Waziri hujasema? nimeshazunguka mikoa yote kasoro Njombe, Ruvuma, Singida na Songwe, kwenye mikoa yote huko nimetoa maelekezo ya kufanyiwa kazi, mojawapo ni dawa za kulevya, amesema Nchemba.
Hata hivyo, Nchemba amesema kuwa akishatoa maelekezo huwa habinafsishi tena shughuli hiyo na kuongeza kuwa mtanzania yeyote anayehusika popote alipo lazima asimamie kwa mapana zaidi, na amewataka wabunge kutoa ushirikiano bila kujali itikadi za vyama.