Mtendaji mkuu wa klabu ya Borussia Dortmund Hans-Joachim Watzke ameionya klabu ya Arsenal, kwa kuitaka ikae mbali na meneja Thomas Tuchel.

Tuchel anatajwa kuwa sehemu ya mameneja wanaofikiria kurithi mikoba ya Arsene Wenger, ambaye mkataba wake utafikia kikomo mwishoni mwa msimu huu.

Watzke amewaambia viongozi wa Arsenal, hakuna haja ya kuanza kumfikiria Tuchel kwa sababu suala hilo halitoweza kuzungumzika.

Alisema: “Hakuna kiongozi yoyote wa Arsenal ambaye ametufahamisha kuhusu uwezekano wa kuondoka kwa Tuchel.

“Tuna mipango mizuri na Tuchel, mwishoni mwa msimu huu tumepanga kukaa nae chini ili kuibua mikakati mipya, ambayo itatuvusha na kuingia katika harakati nyingine za kiushindani, hivyo ni vigumu kukubali kumuachia kwa sasa.”

Kwa upande wa Tuchel amekanusha kuwepo kwa taratibu za kutakiwa na klabu ya Arsenal, aliwaambia waandishi wa habari mwishoni mwa juma: “Unajua mambo mengi kunizidi mimi?. Huwezi kusema chochote kinachonihusu mimi, kwa sababu hujui lolote.

“Nina mkataba wa Dortmund na ninafurahia maisha ya hapa.”

Mkemia Mkuu wa serikali atoa somo kwa wadau
Nape: Tumuunge mkono JPM vita dhidi madawa ya kulevya