Gwiji wa soka nchini Uholanzi Ruud Gullit, ameukosoa uongozi wa klabu ya Leicester City ya England, kwa kuuambia ulipaswa kufanya mabadiliko baada ya kutwaa ubingwa msimu uliopita.

The Foxes wanahaha kujinusuru na janga la kushuka daraja kwa sasa, baada ya kupoteza michezo mitano mfululizo ya ligi ya England, ukiwepo mchezo dhidi ya Swansea City waliochomoza na ushindi wa mabao mawili kwa sifuri.

Gullit, ameuambia uongozi wa klabu hiyo, ulifanya makosa ya kubaki na wachezaji Riyad Mahrez na Jamie Vardy ambao walipata ofa za kutaka kusajiliwa na Arsenal.

“Leicester wameendelea kutumia mfumo kama ilivyokua msimu uliopita, wapinzani wao wameshawasoma na wanatumia makosa yao kuwaadhibu,” Alisema Gulit alipokua akichambua mchezo wa jana kwenye shirika la utangazaji la Uingereza BBC *Match of the Day*.

“Ni makosa makubwa katika soka, mpinzani wako atatambua mbinu zako na kuzitumika kama fimbo ya kukuchapia, tazama mtu kama, (N’Golo) Kante alifanya maamuzi sahihi ya kukubali kuhama, anafanya vizuri akiwa na Chelsea kwa sababu amekutana na mbinu mpya.

“Walipaswa kuwaachia (Vardy na Mahrez), pindi walipopata ofa zao, lakini kitendo cha kuendelea kuwang’ang’ania kilikua ni kosa, kutokana na kocha Ranieri kuamini bado mbinu zake zingefanya kazi kwa kuwategemea.

“Wakati mwingine unatakiwa kubadilika hata ikitokea unashindwa kutetea taji, lakini unakua katika mtazamo mpya wa kiushindani.”

Baada ya mchezo wa jana dhidi ya Swansea City, Leicester City wameporomoka hadi kwenye nafasi ya 17, huku wakiwa na tofauti ya point tatu dhidi ya Sunderland wanaoburuza mkia.

FC Barcelona Ruhsa Kusajili
Miss Kinondoni: Tamaa ya fedha huponza watu maarufu kujihusisha na madawa ya kulevya