Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) amejipanga kuendelea kuendesha mafunzo kwa wadau wa Kanda ya Mashariki wanaohusika na kemikali ili kuhakikisha kemikali zinatumika vema na kwa njia salama.

Hayo yamesemwa leo Jijini Dar es Salaam na Mkemia Mkuu wa Serikali, Prof. Samwel Manyele alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu wasafirishaji na watumiaji wa kemikali nchini.

Amesema kuwa wakala hufanya usajili na ukaguzi kwa wadau wote wanaohusika na kemikali wakiwemo waagizaji, watengenezaji, wasafirishaji, watumiaji, wanaosafirisha nje ya nchi au yeyote yule anayehusika na kemikali kwa njia moja au nyingine.

“Kuanzia mwaka 2012 hadi sasa, wadau wa Mikoa ya Dar es Salaam na Pwani waliopatiwa mafunzo ni 642 wakiwemo Askari wa Jeshi la Polisi Usalama Barabarani Tanzania Bara, wasimamizi wa shughuli za uzalishaji kwenye viwanda, wasambazaji, wasafirishaji wa kemikali pamoja na madereva wanaosafirisha kemikali., hivyo baada ya kuona umuhimu wake tumeamua kuendelea na mafunzo haya kwa wadau wetu wengine,” amesema Prof.Manyele.

Aidha, Wakala Mkuu wa Serikali amefafanua kuwa Wakala hautaruhusu mdau ambaye hajapitia mafunzo hayo kuhusika katika shughuli yoyote ya kemikali kwa kutumia, kuhifadhi, kusafirisha, kutoa bandarini na hata kuagiza kutoka nje ya nchi hivyo akasisistiza umuhimu wa wahusika kuhudhuria mafunzo hayo.

Hata hivyo, ametoa rai kwa wadau hao kuwahi kuhudhuria mafunzo haya ili kutekeleza matakwa ya Sheria Na. 3 ya mwaka 2003 ya Udhibiti na Usimamizi wa kemikali pamoja na kuepuka usumbufu utakaoweza kujitokeza kwa sababu ya kukosa mafunzo

Video: 'Wanaopiga kelele ni wanufaika wa madawa ya kulevya'- Makonda
Watzke: Arsenal Kaeni Mbali Na Thomas Tuchel