Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ilala, Salum Hamdani wamechuana Mahakamani katika kesi ya uchochezi inayomkabili mbunge huyo na wahariri wa gazeti la Mawio.
Hata hivyo, Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba leo anatarajiwa kutoa uamuzi wa kama Hamdani aeleze anachokifahamu juu ya Katiba ya Zanzibar na kama Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha anaweza kufuta matokeo ya uchaguzi.
Hayo yamekuja mara baada ya Lissu kumtaka Hamdani, ambaye ni shahidi wa upande wa mashtaka, kueleze anachokifahamu kuhusu Katiba ya Zanzibar na kama Jecha anaweza kufuta matokeo ya uchaguzi.
Hakimu Simba amefikia uamuzi huo baada ya Wakili wa Serikali, Paul Kadushi kupinga shahidi huyo kujibu swali hilo kwa sababu si mtaalamu wa sheria wala katiba hivyo hawezi kutoa tafsiri ya Katiba ya Zanzibar na kwamba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu haina mamlaka ya kusikiliza masuala ya kikatiba.