Meneja wa mabingwa wa soka nchini Ujerumani FC Bayern Munich Carlo Ancelotti, ameonyesha heshima kwa mpinzani wake Arsene Wenger, kwa kusema mzee huyo wa kifaransa ana uwezo mkubwa wa kupuuza vibweka vya kupingwa.
Ancelotti, alionyesha heshima na Wenger alipokua akizungumzia mchezo wa mkondo wa kwanza wa ligi ya mabingwa barani Ulaya hatua ya 16 bora, ambao utamkutanisha na Arsenal leo usiku mjini Munich.
Anceloti alisema kitendo cha mzee huyo kushindwa kutwaa ubingwa wa nchini England kwa zaidi ya miaka kumi, kimemkomaza kutokana na kelele anazopigiwa kila kukicha na baadhi ya mashabiki wa Arsenal ambao wamechoshwa na hali hiyo.
Ancelotti anaamini Wenger anapaswa kupongezwa kwa jambo hilo, ambalo alisema ni vigumu kwa meneja mwingine kulivumilia.
“Amejenga utambulisho mzuri wa aina ya soka analolifundisha, amejenga himaya ya kuheshimiwa licha ya baadhi ya watu kumbeza kwa kukosa taji la England kwa kipindi kirefu,” Alisema kocha huyo kutoka nchini Italia.
“Wenger ana ujuzi mkubwa katika kazi ya ukocha, anajua nini anachokifanya, japo wakati mwingine ni vigumu kuamini hilo kwa sababu ya kushindwa kufanikia kila inapofika mwishoni mwa msimu, na ndio maana baadhi ya mashabiki wamekua wanampigia kelele.”
“Ninamuheshimu sana kwa kazi kubwa aliyoifanya tangu alipoanza kukinoa kikosi cha Arsenal.”