Meneja wa klabu ya Arsenal Arsene Wenger, amewaomba waandishi wa habari kusitisha maswali kuhusu mustakabali wake ndani ya klabu hiyo, na badala yake kulenga katika changamoto za ushindani wa michezo inayomkabili katika kipindi hiki cha kuelekea mwishoni mwa msimu huu.
Wenger aliwasilisha ombi hilo kwa waandishi wa habari alipokua kwenye mkutano maalum uliozungumzia mchezo wa ligi ya mabingwa barani Ulaya, ambapo hii leo The Gunners watapambana na mabingwa wa soka nchini Ujerumani FC Bayern Munich mjini Munich.
Wenger alisema ni wakati mzuri kwa kila mwandishi kuheshimu kazi inayomkabili kwa sasa, na sio kuangalia mustakabali wake wa baadae.
Kuhusu mchezo wa hii leo, babu huyo wa kifaransa alisema wamejiandaa vyema kupambana, na wametumia makosa yao kushindwa kufurukuta mbele ya Bayern Munich kwa muda mrefu na kuyatumia kama changamoto ya kusaka namna ya kujikwamua.
“Tumekua tukifanya vibaya kila tunapokuna nao, lakini kwa sasa naamini huenda ikawa mwisho wa hadithi hii, tumejiandaa na tumejikita kwenye malengo ya kupata ushindi.” Alisema Wenger.
“Haitopendeza kama tutaendelea kupoteza dhidi yao, itatulazimu kucheza kwa jitihada zetu zote, ili tukamilishe vyema mtihani huu ambao siku zote umekua kikwazo kwa wachezaji wangu kwenye michuano hii.”
“Mchezo huu unanikumbusha namna tulivyoshindwa kusonga mbele mwaka 2013 na 2014.”Tulishindwa kufuzu kwa tofauti ndogo ya mabao na wakati mwingine kanuni ziliwapitisha wapinzani wetu, kwa hiyo ninaamini ni wakati wetu kufanya vizuri.”
Vikisi vya Arsenal na FC Bayern Munich ambavyo huenda vikaanza hii leo.
BAYERN (4-3-3): Neuer; Alaba, Martinez, Hummels, Lahm; Vidal, Alonso, Thiago; Robben, Lewandowski, Muller.
ARSENAL: (4-2-3-1): Ospina; Monreal, Koscielny, Mustafi, Bellerin; Xhaka, Coquelin; Sanchez, Ozil, Walcott; Giroud.
Mwamuzi: Milorad Mazi (Serbia).