Klabu ya Orlando Pirates ya Afrika kusini imemtangaza Kjell Jonevret kuwa kocha mkuu wa klabu hiyo inayoshiriki ligi kuu soka nchini humo.
Kocha huyo raia wa nchini Sweden ametangazwa kuchukua majukumu hayo badala ya Muhsin Ertuğral ambaye alitimuliwa klabuni hapo Novemba mosi mwaka jana, na kwa kipindi chote kikosi cha Orlando Pirates kilikua chini ya kocha wa muda Augusto Palacios.
Jonevret mwenye umri wa miaka 54, atakua na shughuli kubwa ya kuhakikisha anarejesha heshima ya Orlando Pirates ambayo msimu uliopita ilimaliza katika nafasi ya saba kwenye msimamo wa ligi ya Afrika kusini.
Hata hivyo Jonevret anajivunia kuwa na sifa za kipekee za kutajwa kocha bora wa ligi za nchini Sweden na Norway ambazo ziliwahi kuzitumikia akiwa na klabu za huko.
Jonevret, waliwahi kutwaa ubingwa wa ligi ya nchini Sweden akiwa na klabu ya Djurgardens mwaka 2005, na mwaka 2009 alitajwa kuwa kocha bora wa ligi ya Norway akiwa na kikosi cha FK Molde.
Jonevret, amekuja Afrika baada ya kuachana na klabu ya Viking Stavanger ya Norway, aliyoitumikia kwa miaka minne hadi Novemba 2016.