MKurugenzi wa habari na msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbas amewataka maofisa habari na Mawasiliano Serikalini katika mikoa na halmashauri nchini kutumia njia za haraka na za kisasa kwenye mawasiliano ikiwemo matumizi ya tovuti na mitandao ya kijamii ili kutangaza shughuli na mafanikio ya sera na mipango ya serikali kwa wananchi.
Hayo yalisemwa wakati wa uzinduzi wa tovuti za halmashauri 35 za mikoa mitano ya kanda ya Ziwa inayojumuisha Mikoa ya Mwanza, Kagera, Mara, Shinyanga, na Simiyu.
Dkt. Abbas alisema pamoja kuwepo kwa vyombo mbalimbali vya habari vinavyotumika kufikisha taarifa za habari kwa wananchi ikiwemo magazeti na redio, bado mitandao ya kijamii ikiwemo barua pepe imeendelea kutumiwa na wananchi wengi zaidi ulimwenguni kwa sasa.
”Kwa sasa nusu ya watu duniani wapo mtandaoni na hapa nchini kwa mujibu wa ripoti ya TCRA (Mamlaka ya Mawasiliano Nchini) inaonesha kuwa watanzania zaidi ya milioni 19 wapo mtandaoniaidha kwa kutumia barua pepe, au kutembelea kurasa facebook,” amesema Dkt.Abbas.
Dkt. Abbas ameeleza sifa za Ofisa Habari na Mawasiliano wa karne ya sasa ni mwenye uwezo wa kutumia njia za kisasa za mawasiliano, ambazo zitamwezesha kujibu hoja mbalimbali kwa haraka zaidi, badala ya kusubiri serikali kulalamikiwa na wananchi.