Vinara wa ligi kuu ya soka nchini Hispania (La Liga) Real Madrid wameshindwa kufurukuta mbele ya Valencia wanapigania kutokusha daraja msimu huu.
Real Madrid walikubali kupoteza mchezo huo wa kiporo kwa kufungwa mabao mawili kwa moja, na kurejesha ushindani wa kinyang’anyiro cha ubingwa msimu huu dhidi ya FC Barcelona.
Real Madrid walicheza mchezo huo wakiwa na matumaini makubwa ya kuwakimbia zaidi wapinzani wao FC Barcelona lakini imekua tofauti, kwani mpaka sasa wawili hao wanatofautiana point moja.
Real Madrid wapo kileleni kwa kufikisha point 52 na FC Barcelona wakimfuatia kwa kuwa na point 51, lakini The Meringues bado wana faida ya mchezo mmoja mkononi dhidi ya Celta Vigo.
Mabao ya Valencia katika mchezo wa jana yalifungwa na mshambuliaji kutoka nchini Italia Simone Zaza dakika ya nne na Fabian Orellana aliongeza la pili dakika tano baadae huku bao la kufutia machozi la real Madrid likifungwa na Cristiano Ronaldo dakika ya 44.