Klabu ya Blackburn Rovers imemtangaza Tony Mowbray kuwa mkuu wa benchi la ufundi badala ya Owen Coyle aliyefungashiwa virago siku mbili zilizopita.

Mowbray mwenye umri wa miaka 53, amekubali kujiunga na Rovers kwa mkataba wa miezi 18 (mwaka mmoja na nusu), na anatarajiwa kuwa mkombozi wa klabu hiyo inayochungulia kushuka daraja.

Mowbray, msimu uliopita alimaliza mkataba wa kuinoa klabu ya Coventry City, alitarajiwa kuanza rasmi kazi yake hii leo kwa kuongoza mazoezi ya kikosi cha Rovers kwa ajili ya mchezo wa ligi daraja la kwanza utakaochezwa kesho dhidi ya Burton.

Mowbray atasaidiwa na David Lowe ambaye amepandishwa kutoka kwenye kituo cha kulea na kukuza vijana cha Blackburn Rovers, huku gwiji wa klabu hiyo David Dunn akipewa jukumu la kuwa kocha wa kikosi cha kwanza.

Mowbray alianza shughuli za ukufunzi wa soka wakiwa na klabu ya Ipswich Town na kisha alijiunga na klabu nyingine kama Hibernian, West Brom, Celtic, Middlesbrough na Coventry.

Meneja huyo kutoka nchini England atakuwa na kazi kubwa ya kuhakikisha anainusuru Blackburn Rovers katika janga la kushika daraja, ambapo kwa sasa inashika nafasi ya 23 miongoni mwa klabu 24 zinazoshiriki ligi daraja la kwanza.

Paul Stretford Ampigania Rooney, Aelekea Mashariki Ya Mbali
Video: Mauaji ya watu watatu, Waziri Mwigulu atoa tamko