Serikali kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo imetoa agizo kwa wasanii wa hapa nchini kutumia lugha fasaha ya Kiswahili katika kazi zao ili kuitangaza lugha hiyo inayotambulisha Taifa letu.
Agizo hilo limetolewa jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Prof. Elisante Ole Gabriel wakati akizindua program ya kuuza muziki na filamu kwa njia ya mtandao iliyoandaliwa na Kampuni ya Afroprimiere.
Prof. Gabriel amesema kuwa Tanzania inatambulika Duniani kwa lugha ya Kiswahili hivyo wasanii wana nafasi kubwa ya kuendelea kutumia lugha hiyo kwa ufasaha katika kazi zao wanazofanya ili kukuza lugha ya Kiswahili.
“Wasanii mnafanya kazi zenu kwa Kiswahili ni vyema mkatumia lugha hii kwa ufasaha zaidi lakini pia kuweni sehemu ya mafanikio ya mpango huu ili mfanikiwe zaidi.” Amesema Prof. Elisante.
Aidha amewahakikishia wasanii kuwa Serikali itaendelea kutunza haki za wasanii na kuwaunga mkono katika programu hii ili iwe na faida kwa Serikali katika kupata mapato na wasanii pia kupata faida ya kazi zao.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Afroprimiere ambao ndio waandaaji wa program hiyo. Fredy Ngimba amesema kuwa program yao inalenga kuwasaidia wasanii namna wanavyoweza kufaidika na biashara ya kazi zao mtandaoni.
Hata hivyo, Mapato kwa wote wanaohusika katika kazi hiyo yanaonyesha kuwa Msanii ambaye ndio mwenye kazi yake atapata 50%, Muandaaji 25%, Kampuni ya Mawasiliano 20%, mtengenezaji 08% na Serikali 18%.