Wakati Dar24 ikiendelea na kampeni yake ya ‘Shtuka’, iliyolenga kuunga mkono vita dhidi ya dawa za kulevya nchini, ikiwa na kauli mbiu ‘Shtuka Piga Vita Madawa ya Kulevya’, utafiti mpya umegundua athari nyingine kubwa kwa watoto wanaozaliwa na wanaume waliotumia dawa za kulevya hata kama ni baada ya miaka mingi.
Wanaume ambao waliwahi kutumia dawa za kulevya hususani aina ya ‘cocaine’ kabla ya kusababisha ujauzito, wamebainika kuwaathiri kwa kiasi kikubwa watoto hasa wa kiume wanaozaliwa, utafiti umebaini.
Utafiti huo wa hivi karibuni uliofanywa na jopo la wanasayansi kutoka chuo kikuu cha Pennsylvania wakiongozwa na Dkt. Christopher Pierce, umeonesha kuwa watoto hasa wa kiume wa wanaume waliowahi kutumia dawa za kulevya huwa na matatizo ya ubongo yanayopelekea kuwa na matatizo ya uwezo mdogo wa kujifunza na kumbukumbu.
Utafiti huo umebaini kuwa madhara ya dawa za kulevya huwa na athari katika vina saba (DNA) ambazo zinaweza kupitishwa kupitia mbegu za kiume na kuathiri mfumo wa uzazi na kijusi.
Aidha, watafiti hao wamefafanua kuwa athari kubwa zaidi hupatikana kwa watoto wa kiume wa wanaume wanaotumia dawa za kulevya zaidi ya watoto wa kike.
Utafiti huu umejengwa juu ya utafiti wa awali ambao ulionesha kuwa matumizai ya dawa za kulevya aina ya cocaine zina athari kubwa katika vina saba (DNA), ambazo zinaweza kudumu kwa miaka mingi katika damu ya mtumiaji.
Ungana na Dar24 kupitia kampeni ya ‘Shtuka, Piga Vita Madawa ya Kulevya’! Pamoja tunaweza kuliokoa taifa letu dhidi ya mihadarati.