Mmoja wa makocha waliokua wanaunda benchi la ufundi la timu ya taifa ya Ghana wakati wa fainali za AFCON 2017 zilizomalizika mwanzoni mwa mwezi huu nchini Gabon, bado yupo mjini Accra akiishi hotelini kwa kisingizio cha kutaka alipwe mshahara wake.
Gerard Nus ambaye alikuwa msaidizi wa Avram Grant aliyeamua kuachana na Ghana siku chache baada ya kushindwa kufikia lengo la kutwaa ubingwa wa AFCON, amekua akisisitiza kulipwa mshahara wake ili aondoke nchini humo.
Shirika la utangazaji la Uingereza BBC limezungumza na kocha huyo kutoka nchini Hispania na kubaini chama cha soka cha Ghana (GFA) hakijawalipa mishahara watu wa benchi la ufundi ambao walilazimika kuondoka kufuatia maamuzi ya aliyekua bosi wao Avran Grant.
“Inasikitisha kuona hali hii ikiendelea, lakini nitadai haki yangu hadi niipate,” Alisema kocha huyo alipozungumza na BBC Sport.
Gerard Nus
“Kama ilivyo kwa binaadamu wengine, hufanya kazi na mwisho hulipwa mshahara, lakini kwetu imekua tofauti maana hadi suala la kuvunjwa kwa benchi la ufundi kutokana na maamuzi ya Avram Grant kukataa kusaini mkataba mpya, tulikua hatujalipwa pesa zetu na mpaka sasa jambo hilo bado halijatekelezwa.
“Mara kadhaa nimekua ninakumbushia suala la kulipwa pesa zangu, lakini wakati mwingine naambiwa nisubiri maana wanafikiria kunipa nafasi ya kuendelea kuwa sehemu ya benchi lingine la ufundi. Ila jambo kubwa hapa ni kulipwa kwanza mshahara wangu halafu mambo mengine yafatie”
Hata hivyo walipoulizwa GFA kuhusu suala hilo walikiri ni kweli wanadaiwa, lakini wanasubiri fedha kutoka serikalini ili wawalipe makocha ambao walipewa jukumu la kukiogoza kikosi cha Ghana wakati wa fainali za AFCON 2017.