Chama cha Wanasheria Afrika Mashariki (EALS) kimemwandikia barua Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Harrison Mwakyembe kikimtaka aache kuingilia uchaguzi wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS).
Barua hiyo imeandikwa baada ya Dkt. Mwakyembe kudaiwa hivi karibuni kutishia kuifuta TLS kwa madai kwamba imeanza kuingiliwa kisiasa.
Aidha, barua hiyo iliyoandikwa na kusainiwa na Rais wa EALS, Richard Mugisha, imesema TLS si chama cha kisiasa na kimeanzishwa kwa kufuata sheria na taratibu zote.
“Mheshimiwa Waziri, tumesikitishwa na taarifa ambazo zimeenea kwenye vyombo vyote vya habari na gazeti la East African la Februari 18 ambalo limekunukuu ukisema kwamba Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) kina muingiliano wa kisiasa,” imesema sehemu ya barua hiyo.
Katika barua hiyo, Mugisha amesema wanasheria wanatakiwa wapewe uhuru, wasiingiliwe na Serikali kama ilivyo kwa nchi nyingine kwani kuingilia ni sawa na kuvunja sheria za nchi.
Kwa upande wake, rais wa sasa wa TLS, John Seka amesema kuwa chama chake kimefurahishwa na barua hiyo kwa Waziri na kwamba nao pia wanafanya taratibu za kumuona ili kujadili mustakabali wa chama hicho.
Hata hivyo, Uchaguzi wa chama hicho unatarajiwa kufanyika machi 18 mwaka huu, huku wagombea kutoka vyama vya upinzani wakiwa wamejitokeza kuwania nafasi za uongozi wa juu.