Serikali imejipanga kuwatoza kodi wakazi wanaomiliki maeneo yaliyopo mijini ambayo hayana hati wala ofa kwa viwango vile vile ambavyo wakazi wenye hati wanatozwa.
Haya yamesemwa mapema hii leo Jijini Dar es Salaam na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari juu ya ulipaji wa kodi za ardhi.
Lukuvi amesema kuwa Wizara hiyo inaendelea na ukaguzi wa ardhi ambapo mwanzoni ilianza na ukaguzi wa mashamba yanayomilikiwa bila kuendelezwa lakini kwa sasa imegundulika kuwa kuna maeneo makubwa mijini yasiyokuwa na hati yanamilikiwa na wananchi na kusababisha eneo kubwa la ardhi kutumika bila kulipiwa kodi.
“Kwa muda wote huo Serikali imekuwa haiwatozi kodi wananchi wanaomiliki maeneo mijini bila kuwa na hati hivyo, kuanzia sasa Serikali kupitia Wizara yangu itawatoza kodi watu wote nchini wanaomiliki maeneo ndani ya miji hata kama hawana hati au ofa ili mradi wana karatasi za mauziano ya ardhi,”amesema Lukuvi.
Ameongeza kuwa watu wote waliopo mjini ambao wana ardhi lakini hawana hati wala ofa wapeleke taarifa zao za maeneo wanayoyamiliki kwa maafisa wateule wa ardhi kwenye halmashauri zao ili yaweze kujulikana ili kuanza kulipiwa kodi.
Aidha, Lukuvi amesema kuwa kuanzia mwezi Julai mwaka huu Wizara itaanza kuwatoza kodi wananchi wote waliojenga mjini katika maeneo ambayo viwanja vyake havijapangwa wala kupimwa kwani watu hao wanaishi mjini na wanatumia miundombinu ya umma inayojengwa kwa kutumia kodi za wananchi.
Hata hivyo, Lukuvi amesema kuwa ni lazima kuwatambua watu wote wanaomiliki ardhi kisheria, kimila au kwa namna nyingine yoyote ili kufahamu ardhi inamilikiwa na nani na inatumika kwa matumizi gani.