Klabu za Liverpool na Man City zimetakiwa kukaa mbali na beki Virgil van Dijk, baada ya kuhusishwa na mpango wa kutaka kumsajili itakapofika mwishoni mwa msimu huu.
Mwenyekiti wa klabu ya Southampton Ralph Krueger ametuma salamu hizo Etihad Stadium na Anfield kwa kuamini huenda zikasaidia kuepusha usumbufu ambao huenda ukajitokeza wakati wa majira ya kiangazi.
Beki huyo mwenye umri wa miaka 25, amekua katika mawindo makali ya Liverpool, Man City na Paris St Germain kwa kipindi kirefu na wakati wa majira ya baridi (Dirisha dogo la usajili) zilijaribu kumsajili lakini ilishindikana.
Akizungumza na vyombo vya habari baada ya kikosi chake kushindwa kutwaa ubingwa wa kombe la ligi (EFL Cup), kwa kufungwa na Man Utd mabao matatu kwa mawili mwishoni mwa juma lililopita, Krueger alisema hawatopokea ofa yoyote itakayomuhusu beki huyo.
“Virgil ni mchezaji anaejua majukumu yake na amekua kiongozi mzuri kwa wenzake, na ndio maana amepewa unahodha, sitarajii kuona vurugu za usajili dhidi yake mwishoni mwa msimu huu,”
“Najua Liverpool na Man City zimeanza kupigana vikumbo kwa mara nyingine tena, ili kuangalia uwezekano wa kumsajili, lakini ninawaambia viongozi wao kuwa, Virgil hauzwi.”
“Hatutaki kurudia makosa tuliyoyafanya miaka mitatu iliyopita, kwa kukubali kuwaachia kirahisi wachezaji wetu, tumedhamiria kuwa na kikosi bora, na tunaamini tukiendelea kukaa na wachezaji waliopo sasa, itatuchukua muda mfupi kupata mafanikio.”Alisema Krueger.