Malkia wa ‘Talk Show’ anayetajwa kuwa moja kati ya wanawake maarufu zaidi duniani, Oprah Winfrey ameanza kuuwaza urais wa Marekani na huenda akajiingiza katika mbio za uchaguzi wa rais mwaka 2020.
Akifunguka katika uzinduzi wa msimu wa pili wa ‘The David Rubenstein Show: Peer to Peer Conversations’ inayorushwa kupitia kituo cha runinga cha Bloomberg, Oprah alieleza kuwa awali alikuwa hajawahi kufikiria kama siku moja atakuwa na wazo hilo, lakini sasa mambo yamebadilika.
Oprah aliungana na mtangazaji wa kipindi hicho kuwa hivi sasa mambo yamebadilika kwa sababu imeonesha dhahiri kuwa uzoefu serikalini sio kigezo cha kuwa rais wa taifa hilo kubwa na lenye nguvu zaidi duniani.
“Sikuwahi kuwaza kwamba… sikuwahi kufikiria kuhusu swali hilo. Hata uwezekano tu, nilikuwa nadhani…oh, oh…! Lakini sasa nafikiria kama…oh, oh” alisikika, kabla ya kuunga na wazo la mtangazaji huyo aliyesema, “Kwa sababu iko wazi hivi sasa kwamba hauhitaji kuwa na uzoefu serikalini kuchaguliwa.”
Ingawa Oprah hakutaja jina, alionesha kurejea hali ya nchi hiyo kumchagua mfanyabiashara Donald Trump kuwa Rais wa nchi hiyo ingawa hakuwa na uzoefu wa nafasi ya uongozi Serikalini.