Mwimbaji mwenye kiuno bila mfupa, Shakira amefunguliwa kesi ya madai katika mahakama ya Hispania kwa tuhuma za wizi wa baadhi ya mashairi yanayosikika kwenye wimbo wake wa ‘La Bicicleta’ aliofanya  na Carlos Vives.

Wimbo huo ulishinda tuzo ya Grammy mwaka jana kama wimbo bora zaidi wa mahadhi ya ‘Kilatino’.

Kesi hiyo imefunguliwa mahakamani hapo na mwimbaji kutoka Cuba, Livan Rafael ambaye amedai kuwa Shakira na Vives walinakili bila ruhusa yake baadhi ya mistari na sehemu ya wimbo wake wa mwaka 1997 unaojulikana kama ‘Yo Te Quiero Tanto’.

Msemaji wa mahakama hiyo ya Uhispania ameviambia vyombo vya habari kuwa kesi iliyofunguliwa mahakamani hapo ni ya wizi wa kazi ya sanaa na kwamba cha msingi ni ‘melodi’ na mashairi ya kiitikio vinavyoonesha mfanano kwa nyimbo zote mbili.

Gazeti la Uhispania la El Mundo liliandika kuwa pande zote mbili ziliwahi kukutana mwezi Oktoba mwaka jana kujaribu kuumaliza mgogoro huo lakini hawakufanikiwa kufikia muafaka.

Shirika la habari la AFP limeeleza kuwa kambi ya Shakira ilipofikiwa ilikataa kuzungumzia suala hilo.
Angalia nyimbo zote mbili, je, ni kweli zinamfanano?

Magufuli: Serikali haitatoa msaada wa chakula
Atletico Madrid: Torres Anaendelea Vizuri