Klabu ya Atletico Madrid imetangaza maendeleo ya mshambuliaji Fernando Torres kwa kusema yupo vizuri, baada ya kukimbizwa hospitali usiku wa kuamkia hii leo.
Torres alipata majeraha ya kichwa akiwa kwenye mchezo wa ligi ya nchini Hispania ambapo Atletico Madrid walikuwa wageni wa Deportivo La Coruna na waliambulia matokeo ya sare ya bao moja kwa moja.
Mshambuliaji huyo wa zamani wa Liverpool na Chelsea zote za England, alipatwa na mkasa huo katika dakika ya 85 alipokua akikabiliana na Alex Bergantinos.
Baada ya kutokea tukio la kugongana, Torres alipoteza fahamu na watoa huduma ya kwanza walilazimika kumkimbiza hospitali kwa ajili ya kupatiwa matibabu zaidi.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari baada ya mchezo huo, meneja wa Atletico Madrid Diego Simeone, alisema aliogopa kuona tukio hilo, kwa sababu hakulitarajia.
Alisema ni nadra sana kuona mshambuliaji akipoteza fahamu uwanjani na kukimbizwa hospitali, hivyo tukio hilo lilipotokea alifikia mbali na kuogopa.
Tukio la kuumia kwa Torres, liliisababishia Atletico Madrid kucheza pungufu kwa zaidi ya dakika 5 za mwisho, baada ya meneja Simione kumaliza idadi ya wachezaji watatu wa akiba.
Katika mchezo huo Deportivo La Coruna walitangulia kupata bao la kuongoza katika dakika ya 13 kupitia kwa Florin Andone, lakini dakika ya 68 mshambuliaji Antoine Griezmann aliisawazishia Atletico Madrid.