Kwa kipindi kirefu kulikuwa na moshi mweusi wa tetesi zilizosambaa mtaani kuwa kuna ‘bifu’ kati ya Fid Q na Joh Makini, tetesi zilizoishi miaka mingi kabla hazijazikwa hivi karibuni baada ya Ngosha kupost video ya Mweusi Joh ‘Waya’.
Leo, Ngosha amefunguka kilichotokea kuhusu tetesi hizo ambazo amedai zilipikwa na mashabiki kwa sababu zao.
Akifunguka leo kwenye The Playlist ya 100.5 Times FM inayoongozwa na Lil Ommy, Ngosha ambaye amekana kuwahi kuwa na tofauti yoyote na Joh Makini, amesema kuwa anadhani tetesi za bifu kati yao zilipikwa na mashabiki ambao walitamani apate mshindani (challenger) kati ya waliokuja baada yake.
“Nafikiria wasikilizaji walivyo, kama mtu alikuwa mkali huwa wanamtafutia challenger (mshindani) wa yule mkali wao wa siku zote. Nafikiri ndio maana walianza kutengeneza competition (mashindano) yao wenyewe ambayo wanayajua wao wenyewe na kwa sababu zao wao wenyewe,” Ngosha anafunguka.
“Lakini kibinadamu na kimaisha mengine nje ya muziki mimi sina shida na jamaa yeyote,” aliongeza rapa huyo anayetajwa kuwa tajiri wa mashairi na ‘flow’.
Katika hatua nyingine, Fid Q alifunguka kwa mara ya kwanza kuwa ingawa hajawahi kuwa na mawasiliano ya karibu na Joh Makini, yeye ndiye aliyempa mchongo wa kuingia ‘Coke Studio’ akiwa kama rapa pekee kutoka Tanzania.
Fid alisema kuwa awali alipigiwa simu na watu wa Coke Studio kumtaka ashiriki lakini kutokana na kuwa mbali pamoja na muingiliano wa ratiba, hakuweza. Hivyo, alimpendekeza Joh Makini kuwa ndiye anayeweza kufanya vizuri kwa wakati huo.
Hata hivyo, anasema hakuwahi kumueleza Joh kama yeye ndiye chanzo cha mchongo huo.
“Coke studio walipokuwa wanatafuta mtu wa kurap au mtu wa hip hop, sura ya Fid Q ndio iliyomjia ya kwanza bwana Bless (Mratibu wa Coke Studio), akanivutia waya lakini akanikuta mimi niko tight, ratiba imebana na siwezi kusafiri. Mimi nikam-recommend Joh,” alifunguka.
“Hata hivyo, sikuwa na namba ya Joh, ikabidi nimpe namba ya G-Nako. Kwahiyo, hivi ni vitu ambavyo watu hawajui na nina uhakika hata Joh mwenyewe anaweza kuwa hata hajui,” aliongeza.
Alisema aliamchagua Joh Makini baada ya kuangalia sifa walizokuwa wanazitaka watu wa Coke Studio akaamini rapa huyo kutoka Arusha hatatuangusha.