Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ametoa agizo kwa uongozi wa tanesco kukata umeme kwa Wizara au taasisi yoyote inayokwepa kulipa bili za umeme.
Rais ameyasema hayo katika ziara yake ya kuzindua na kuweka jiwe la msingi katika mradi wa umeme wa msongo wa Kv 132 Mtwara, amesema ili nchi iendelee lazima taasisi na Wizara mbalimbali zilipe bili ya umeme.
“Tanesco pasitokee taasisi ama Wizara hata Ikulu isipolipa umeme we kata tu, hatuwezi kujiendesha kwa hasara wakati kuna watu wanakwepa kulipia gharama, wakati Serikali inatoa ruzuku zake humu sasa ni wakati Tanesco ijiendeshe kwa faida,”amesema Rais Magufuli.
Hata hivyo, Rais Magufuli ameionya Tanesco kutoingia mikataba ya hovyo na makampuni ya nje yanayokuja kwa ujanja ujanja na kuongeza kuwa Kampuni ikitaka kuja kuwekeza umeme nchini basi waje wazalishe umeme wao na waiuzie Tanesco, na wasitegemee umeme huu kufanya ujanja ili kutorudia mikataba mibovu kama Symbion na makampuni mengine.