Ikiwa ni zaidi ya mwaka mmoja tangu Serikali ilifungie milele gazeti la Mawio, Mahakama Kuu nchini imeamuru kuwa uamuzi huo haukuwa sahihi.

Uamuzi huo wa Mahakama Kuu umetolewa wiki iliyopita na jopo la majaji watatu lililoongozwa na Jaji Sakieti Kihiyo ambapo jopo hilo limeeleza kuwa gazeti hilo lilifungiwa bila kupewa nafasi ya kujitetea.

Akizungumzia hatua hiyo ya Mahakama, Mkurugenzi Mtendaji wa Mawio, Simon Mkina amesema kuwa kutokana na uamuzi huo wa Mahakama, gazeti hilo litarejea mtaani Alhamisi wiki hii.

“Kwa muda zaidi ya mwaka mmoja, gazeti wakati halipo mtaani baada ya kufutwa na Serikali, pamoja na kupoteza ajira za watu na kuingia katika hasara kubwa, tulikuwa tukijiuliza ni wapi tumekosea?” Mkina anakaririwa na MwanaHalisi na kudai kuwa walikuwa wakisubiri kupata haki yao.

Wachapishaji wa gazeti hilo ambao ni Kampuni ya Victoria Media Services Limited, walifungua kesi mahakamani kupinga uamuzi wa kufungiwa ambapo walikuwa wakitetewa na Wakili, Dkt. Rugemeleza Nshalla.

Januari 15 mwaka jana, Serikali kupitia notisi namba 55 ya mwaka 2016 ilitangaza kulifungia gazeti hilo kwa muda wote kwa kile kilichoelezwa kuwa limekuwa likichapisha habari za kichochezi. Serikali ilichukua uamuzi huo kwa mujibu wa Sheria ya Magazeti ya Mwaka 1976, Sura ya 229, kifungu cha 25 (1).

Sakata la kufungiwa kwa gazeti hilo lilianza Desemba mwaka 2015, baada ya Msajili wa Magazeti kumuandikia barua mhariri wa gazeti hilo kujieleza kwanini gazeti hilo lisifungiwe kwa kuandika habari za uchochezi na zilizodaiwa kuzua taharuki.

Chanzo: MwanaHalisi

Mchakato wa utafutaji Gesi na Mafuta kuanza Visiwani Zanzibar
JPM aagiza Dangote apewe eneo la kuzalisha makaa ya mawe