Hatimaye kazi ya utafutaji wa mafuta na gesi asilia Visiwani Zanzibar inatarajia kuanza wakati wowote kuanzia sasa kwa kutumia ndege maalumu katika maeneo ya nchi kavu na bahari.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira wa Zanzibar, Salama Aboud Talib, amesema kuwa kazi ya awali ya utafutaji itaanza kwa kitalu cha Pemba.
“Taarifa hii inakusudia kuwajulisha wananchi wote wa Unguja na Pemba kuwa hivi karibuni kazi ya awali ya itaanza,” amesema Talib.
Waziri huyo amebainisha kuwa utafutaji huo utafanywa na Kampuni ya Bell Geospace Enterprises ya Uingereza ikitumia vifaa mbalimbali ikiwemo ndege kukagua miamba iliyoko chini ya ardhi na baharini.
Aidha, Salama amesema hatua ya kwanza ya utafiti itachukua miezi minne na Serikali inawaomba wananchi wasiwe na hofu wakati kazi hiyo ikiwa inaendelea kwa kuwa hakutakuwa na athari zozote.
Hata hivyo, Kuanza kwa kazi ya utafutaji wa mafuta na gesi asilia kunaanza baada ya Rais wa Zanzibar, Dkt. Ali Mohamed Shein kutia saini Sheria ya Utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta na Gesi Asilia mwezi Novemba, mwaka jana.