Rais wa chama cha soka nchini Djibouti, Souleiman Hassan Waberi ameungana na baadhi ya mataifa ya bara la Afrika yanayomkubali mgombea nafasi ya urais wa CAF kutoka Madagascar, Ahamd Ahmad.

Maamuzi ya Waberi yanakwenda kinyume na marais wa vyama vya soka ukanda wa mashariki mwa Afrika ambapo kwa pamoja walikubaliana kumuunga mkono rais wa sasa wa CAF, Issa Hayatou anaewania kiti hicho kwa mara ya nane mfululizo.

“Sisi kama Djibouti tunataka kuona mabadiliko katika soka la Afrika, tutahakikisha tunakwenda kumchagua Ahmad. Tutapiga kura kwa ajili ya mabadiliko kama ilivyokua wakati wa uchaguzi wa urais wa FIFA ambapo asilimia kubwa tulimchagua Gianni Infantino,” Waberi anakaririwa na BBC.

Hata hivyo, kiongozi huyo ameomba asionekane kama msaliti dhidi ya wanachama wengine wa baraza la vyama vya soka ukanda wa mashariki mwa Afrika (CECAFA), kwa kusema maamuzi aliyoyachukua ni kwa ajili ya kuona Afrika inabadilika.

Mwishoni mwa juma lililopita rais wa shirikisho la soka nchini Uganda, Moses Magogo alishindwa kuwathibitishia waandishi wa habari ni wapi atakapoiweka kura yake lakini alitoa ahadi ya kuachiwa jambo hilo hadi siku chache kabla ya uchaguzi wa urais wa CAF.

Magogo alihojiwa na vyombo vya habari kuhusu uamuazi wake wa kupiga kura, wakati wa ziara ya rais wa shirikisho la soka duniani FIFA Gianni Infantino alipotembelea nchini Uganda.

Ukanda wa soka mashariki mwa Afrika (CECAFA) una nchi wanachama 11 ambao ni Djibouti, Sudan, South Sudan, Uganda, Burundi, Tanzania, Rwanda, Somalia, Eritrea, Ethiopia na Kenya.

Ahmad ambaye pia ni rais wa chama cha soka nchini Madagascar tayari ameshapata uhakika wa kura za ukanda wa kusini mwa Afrika (COSAFA), huku rais wa shirikisho la soka nchini Nigeria Amaju Pinnick akithibitisha kuwa pamoja na mgombea huyo.

Uchaguzi wa rais wa CAF umepangwa kufanyika Machi 16 mjini Adis Ababa nchini Ethiopia.

Issa Hayatou, alianza kuliongoza shirikisho la soka barani Afrika tangu mwaka 1988.

Kumbe Wenger Ana Ugomvi Na Alexis Sanchez!
Lema ampa somo Wema, amtaka awe na ndoto hata ya Urais