Beki wa klabu ya Olympic Lyon ya Ufaransa, Nicolas Alexis Julio Nkoulou Ndoubena ameomba kupumzika kwa muda kuitumikia timu ya taifa ya Cameroon ambayo juma lijalo itacheza michezo ya kumataifa ya kirafiki.

Nkoulou ambaye alifunga bao la kusawazisha wakati wa mchezo wa fainali ya michuano ya Afrika dhidi ya Misri mapema mwezi uliopita, amewasilisha ombi hilo kwenye ofisi za shirikisho la soka nchini Cameroon FECAFOOT.

Beki huyo mwenye umri wa miaka 26 wamewaarifu viongozi wa FECAFOOT kuhusu maamuzi hayo, kwa kubainisha hana nia mbaya ya kufanya hivyo, bali anaamini kipindi hiki ni kuzuri kwake kupumzika kwa muda kabla ya kurejea tena kuitumikia Cameroon siku za usoni.

“Baada ya kufanya kazi kubwa ya kuiwezesha nchi yangu kutwaa ubingwa wa Afrika mwezi uliopita, nimeomba kupumzika kwa muda ili nifanikishe mpango wa kufanya mambo mengine, lakini ninasisitiza nitarudi na kujiunga na wenzagu mara baada ya michezo ya kimataifa ya kirafiki itakayochezwa juma lijalo,” imeeleza taarifa ya Nkoulou aliyoiwasilisha FECAFOOT.

“Tangu nilipoanza kuvaa jezi za timu yangu ya taifa mwaka 2008, sikuwahi kupumzika, nimecheza kwa kipindi kirefu kwa moyo wote, sasa ni muda mzuri wa kuomba kupumzika kwa siku chache kabla ya kuendelea kulitetea taifa langu hapo baadae.”

“Maamuzi haya sio rahisi kuyachukua, kwa sababu natambua baadhi ya wadau watayapokea kwa mtazamo tofauti, lakini ninaendelea kusisitiza nimefanya hivi kwa lengo zuri na wala sina nia mbaya ya kwenda kinyume na matarajio ya soka la Cameroon.”

Mpaka sasa Nkoulou ameshaitumikia timu ya taifa ya Cameroon katika michezo 75, na kufunga mabao mawili.

Mongela awataka wanawake kushiriki katika shughuli za kisiasa
Tanesco kuweka hadharani deni la Zanzibar