Wanafunzi wa shule ya sekondari ya Bariadi iliyopo katika halmashauri ya mji wa Bariadi Mkoani Simiyu wameandamana na kufunga barabara kuu ya Bariadi –Lamadi kupinga kuhamishwa kwa mkuu wa shule hiyo, Deus Toga.
Wanafunzi hao walianza kuandamana kuelekea katika ofisi ya mkurugenzi wa halmashauri, lakini ilishindikana baada ya kikosi cha jeshi la polisi cha kuzuia ghasia (FFU) kuwazuia kwenda katika ofisi hizo.
Wanafunzi hao wakiwa katikati ya barabara hiyo waliamua kuandamana tena kuelekea katika ofisi ya mkuu wa mkoa jambo lililoshindikana pia baada ya askari hao kuwazuia tena eneo la Hospitali teule ya mkoa (Somanda), ndipo wakaamua kukaa katikati ya barabara huku wakiimbanyimbo za kushinikiza kuwa hawamtaki mwalimu, Paul Lutema ambaye alikuwa amepelekwa kuwa mwalimu mkuu wa shule hiyo.
“Hatumtaki mwalimu Lutema……tunamtaka mwalimu wetu Toga…..hatumtaki Lutema……Tunamtaka mwalimu Toga” waliimba wanafunzi hao
Kufuatia hali hiyo, Kiongozi wa chama cha ACT-Wazalendo na Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe amewapongeza wanafunzi hao kwa kitendo hicho cha kuandamana kudai haki yao wakitaka mwalimu mkuu wao kurejeshwa Shuleni hapo.
Aidha, Zitto amelilalamikia jeshi la polisi, ambapo ameeleza kuwa lilipaswa kutoa ulinzi kwa wanafunzi hao na sio kuwapiga kama wahalifu.
“Nawapongeza Sana Wanafunzi wa Bariadi walioandamana kudai haki yao ya Mwalimu Mkuu wao kurejeshwa shuleni hapo. Jeshi la Polisi lilipaswa kutoa ulinzi kwa Wanafunzi hawa na sio kuwapiga kama wahalifu. Wezi kama kina Harbinder Singh Seth wa PAP/IPTL wanapewa ulinzi wa polisi na usalama wa Taifa wakati watoto wanaodai haki ya Mwalimu bora wanapigwa.”
Zitto amesema hayo kupitia ukurasa wake wa facebook leo Machi 7, 2017, ambapo amesema kuwa OCD wa Bariadi na RPC wa Simiyu wapaswa kuwajibishwa kwa kutumia nguvu kubwa dhidi ya Wanafunzi hawa.
“OCD wa Bariadi na RPC wa Simiyu wawajibishwe kwa kutumia nguvu kubwa dhidi ya Wanafunzi hawa.
Nawashawishi Mtandao wa Wanafunzi Tanzania ( TSNP ) kuhamasisha Wanafunzi nchi nzima waandamane kulaani wanafunzi wenzao kupigwa na polisi huko Bariadi mkoani Simiyu” Amesema Zitto Kabwe