Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) inategemea kukabidhi jumla ya shilingi bilioni 568.575, 000/= kwa vijana 12 waliobuni mawazo bora yatakayosaidia kuondoa changamoto zinazoikabili sekta ya Afya hapa nchini.
Mkurugenzi wa Tume ya Sayansi na Teknolojia, Dkt. Hassan Mshinda ameyasema hayo Jijini Dar es Salaam alipokuwa akizindua mradiwa Data for Local Impact Innovation Challenge (DLI) uliopo chini ya Atamizi ya DTBi yenye lengo la kuleta mapinduzi katika matumizi ya taarifa na takwimu mbalimbali katika sekta ya Afya.
Dkt. Mshinda amesema shughuli za ujasiriamali na ubunifu ni muhimu na chachu ya maendeleo ya nchi yoyote kwa kuwa zinasaidia kutengeneza ajira, kuongeza wigo wa shughuli za uzalishaji mali pamoja na kuchangia katika pato la taifa.
Amesema Serikali kupitia COSTECH iliamua kuanzisha Atamizi ya DTBi mwaka 2011 ili kuwasaidia wajasiriamali wanaoshughulika na suala la TEHAMA.
“Nafahamu mradi huu umejikita katika changamoto za matumizi ya taarifa katika sekta ya afya, maendeleo ya kiuchumi na usawa wa kijinsia kama yalivyotanabaishwa katika malengo ya maendeleo endelevu, ubunifu hasa katika eneo la TEHAMA ni muhimu sana kwa sababu unasaidia kuongeza tija na ufanisi wa utoaji huduma katika sekta mbalimbali nchini”,Amesema Dkt. Mshinda.
Aidha Dkt. Mshinda amesema nia ya DTBi ni kuwawezesha Vijana, kuwajengea uwezo na kuwapa misaada ya msingi wataalam na wabunifu wa kitanzania waliopo katika eneo la TEHAMA ili kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii ya kitanzania kwa kutumia teknolojia.
Kwa upande wake Meneja Mradi wa DTBi, Agapiti Manday amesema wanapokea mawazo mbalimbali ya vijana na kuyachuja na baadae wanachukua vijana wachache walio na mawazo bora zaidi na kuwawezesha ili waweze kuweka mawazo yao katika vitendo.
Mradi huo mpya kwa Tanzania, umefadhiliwa na Mfuko wa Rais wa Marekani katika Vita dhidi ya Makali ya UKIMWI (PEPFAR) na kusimamiwa na taasisi ya serikali ya marekani ya Changamoto za Millenia (MCC), Mradi huu umeanza utekelezaji mnamo mwezi Aprili mwaka 2016.