Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) na Bodi ya Nyama Tanzania (TMB) zimejidhatiti kusaidia mnyororo wa thamani wa ufugaji wa ng’ombe wa nyama na maziwa ili kuongeza tija kwenye sekta ya ufugaji wa ng’ombe nchini.
Hayo yamesemwa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Francis Assenga na Afisa Masoko na Utafiti, Nicholas Chiweka kutoka TMB wakati wa majadiliano kuhusu Mkutano Mkuu wa Wadau wa Bodi ya Nyama utakaofanyika mkoani Dodoma kuanzia tarehe 8 hadi 9 Machi, 2017.
Assenga amesema kuwa TADB imejidhatiti katika kuongeza tija kwa Ufugaji wa Ng’ombe wa Nyama na Maziwa kwa kutoa mikopo na kusaidia shughuli mbali mbali za uongezaji tija wa ufugaji huo.
“Katika kuhakikisha sekta hii inaendelea na kuongeza tija, TADB imejipanga kutoa mikopo itakayotumika kama mtaji kwa ajili ya uendeshaji wa mashamba, uongezaji wa thamani na gharama za uhifadhi wa nyama/maziwa na miundombinu masoko kwenye sekta hii,” amesema Assenga.
Ameongeza kuwa kwa kushirikisha wadau wa Kilimo, utafiti, huduma za ugani na madaktari wa mifugo TADB imelenga kuwapatia wafugaji mafunzo ya ufugaji wa kisasa wa ng’ombe wa nyama na maziwa kwa kutumia mbinu bora za ufugaji ili kufuga kibiashara na hivyo kujiongezea kipato na kupambana na umaskini.
Kwa upande wake Afisa Masoko na Utafiti, Nicholai Chiweka kutoka TMB amesema kuwa TMB ina Mamlaka yenye dhamana ya kusimamia maendeleo ya tasnia ya nyama, iliyoanzishwa kwa Sheria ya Nyama Na. 10 ya Mwaka 2006 hivyo ina wajibu wa kuratibu mnyororo mzima wa thamani wa tasnia ya nyama na kuiomba TADB kushirikiana na TMB kunyanyua sekta ya nyama.
“Kifungu Na. 17 (1) cha sheria hii, kinazuia mtu yeyote kufanya shughuli ya aina yoyote katika tasnia ya nyama bila ya kuwa na cheti cha usajili kutoka Bodi ya Nyama Tanzania hivyo kama mdau wa kuendeleza sekta hii tunaiomba TADB kuwasaidia wadau wa mnyororo mzima wa thamani wa tasnia ya nyama ambao wamesajiliwa na TMB,” amesema Chiweka.