Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa ameutaka uongozi wa Wakala wa Ufundi na Umeme nchini (TEMESA) kushiriki kikamilifu shughuli za matengenezo ya vivuko ili kupata ujuzi wa ufungaji wa mifumo kutoka Kampuni zinazotengeneza vivuko vya Serikali.
Ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kufanya ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi wa kivuko kipya cha MV Kazi, Bandarini jijini Dar es Salaam, Prof. Mbarawa amesema kuwa kupitia mafunzo hayo Serikali itaweza kuokoa fedha nyingi ambazo kwa sasa inatumia kulipa kampuni binafsi zinazojenga na kukarabati vivuko.
“Hakikisheni mnapata ujuzi kama walionao hawa, hatutaki kutumia fedha za Serikali kwa ajili ya kukarabati au kutengeneza vivuko wakati nyinyi TEMESA mpo”, amesema Prof. Mbarawa.
Aidha, Prof. Mbarawa ameuagiza Wakala huo kuhakikisha wanakamilisha mifumo ya ukusanyaji mapato kwa njia ya kielektroniki ili kudhibiti mianya ya rushwa.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Wakala huo Dkt. Musa Mgwatu, amemtaka mkandarasi wa kampuni ya Songoro Marine Transport kuhakikisha anafanya kazi usiku na mchana ili kukamilisha kivuko hicho kwa muda uliopangwa.
Naye, Meneja Mradi wa Kampuni ya Songoro Marine Transport, Major Songoro amemhakikishia Waziri Mbarawa kumaliza kivuko hicho kwa wakati ambapo amesema ifikapo tarehe 15 mwezi huu kivuko hicho kitakabidhiwa kwa Serikali.
Hata hivyo, Kivuko kipya cha MV Kazi kimegharimu kiasi cha shilingi bilioni Saba na kina uwezo wa kubeba abiria 800 na magari 22 kwa wakati mmoja.