Meneja wa Arsenal Arsene Wenger, amewataka mashabiki wa klabu hiyo kutowalaumu wachezaji na badala yake wazigeuzie lawama hizo kwa mwamuzi aliyechezesha mchezo wa kuamkia leo dhidi ya FC Bayern Munich.
Wenger aliwaambia waandishi wa habari baada ya mchezo huo kumalizika kwa mabingwa wa soka nchini Ujerumani FC Bayerrn Munich kupata ushindi wa mabao matano kwa moja kwenye uwanja wa Emirates.
Wenger alisema mwamuzi hakuitendea haki Arsenal kwa kufanya maamuzi ya kumuonyesha kadi nyekundu Laurent Koscielny huku ikiwa tayari alikua ameshamuonyesha kadi njano baada ya kufanya kosa la kumvuta mshambuliaji wa FC Bayern Munich Robert Lewandowski.
Alisema makosa yalianzia hapo, na ndipo wapinzani wao walipata mwanya wa kuwashinda kirahisi kwa kupata ushindi mnono wa mabao matano kwa moja.
Katika mchezo huo Arsenal walitangulia kupata bao lilifungwa na mshambuliaji Theo Walcott katika dakika ya 20, na wapinzani wao walisawazisha bao hilo kupitia kwa Robert Lewandowski kwa njia ya penati dakika ya 55.
Baada ya hapo mvua ya mabao ikaanza kuinyeshea Arsenal kupitia kwa Arjen Robben, Douglas Costa na Arturo Vidal aliyefunga mabao mawili.
Kwa mantiki hiyo Arsenal wametupwa nje ya michuano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya msimu huu, kwa kukubali kufungwa jumla ya mabao kumi kwa mawili.