Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani amezindua rasmi mradi wa usambazaji wa umeme vijijini unaotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Awamu ya Tatu kitaifa kwa kushirikiana na Shirika la Umeme nchini Tanesco, utakao sambaza umeme kwa vijiji vyote ambavyo havikupata huduma hiyo wakati wa REA Awamu ya Kwanza na ya Pili.
Dkt . Kalemani amesema kuwa REA Awamu ya Tatu itatekelzwa kwa miaka mitano kuanzia sasa hadi kufikia 2021, na kufafanua kuwa mara baada ya uzinduzi rasmi wa kitaifa wa mradi huo mkoani Tanga, Mikoa mingine itaendelea kuzindua mradi huo katika mikoa yao kulingana na makubaliano ya mikataba ya wakandarasi husika katika Mikoa hiyo.
“REA awamu ya Tatu imezinduliwa rasmi hapa mkoani Tanga, mradi huu sasa utamaliza kazi ya kuunganisha huduma ya umeme katika vijijini vyote 7867 nchini vilivyoachwa katika Awamu ya Kwanza na ya Pili ya mradi huo, ili kifikia idadi ya vijiji vyote 12,262,Tanzania bara ifikapo mwaka 2021”, alisema Kalemani.
Dkt. Kalemani amesema kuwa REA Awamu ya Tatu itasambaza huduma ya umeme katika vijiji 166 mkoani Tanga, ambapo vijiji 20 kati ya hivyo ni vile ambavyo vilipitiwa na Mradi wa REA Awamu ya Kwanza na ya Pili lakini havikuunganishwa na huduma ya umeme , na vijiji 146 ambavyo havikupitiwa kabisa wala kuunganishwa na Mradi wa usambazaji wa umeme vijijini iliyopita.
Pia ametoa wito kwa wakandarasi watakaotekeleza Mradi wa REA Awamu ya Tatu, kutekeleza majukumu yao kwa wakati kwa kuzingatia uhitaji wa huduma ya umeme nchini ili kutimiza azma ya Serikali ya kuwa nchi ya viwanda.
Akizungumza Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martin Shigela amewataka wakazi wa Mkoa huo waliokosa huduma hiyo katika miradi iliyotangulia, kutandaza nyaya za umeme katika nyumba zao ili kuweza kuunganishwa na huduma ya umeme ambayo hupatikana kwa bei nafuu ya shilingi elfu 27 .
Shigela amewataka wananchi hao kulinda na kuitunza miundombinu ya mradi huo kwa maslahi ya taifa na wananchi kwa ujumla kwa kuwa miundombinu hiyo ni ya gharama kubwa.