Mkuu wa Wilaya ya Temeke Felix Lyaniva amevitaka vikundi vya VICOBA kujisajili mapema iwezekanavyo ili viweze kutambulika na kupata uwezeshaji kiuchumi.

Lyaniva amesema hayo leo Machi 8, 2017 jijini Dar es Salaam katika maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, ambapo ameeleza kuwa vikundi vya VICOBA vilivyopo ni takribani 2748 lakini kati ya hivyo vilivyosajiliwa na kutambulika ni 746, hivyo vikundi 2200 havijasajiliwa, hivy0 ni vyema vikasajiliwa haraka iwezekanavyo ili viweze kupata fursa hiyo adhimu ya uwezeshaji kiuchumi.

Lyaniva amesema kuwa Machi 20 mwaka huu kutakuwa na jukwaa la uwezeshaji wanawake katika uwanja wa Mnazi Mmoja ambapo mgeni rasmi atakuwa Makamu wa Rais, Samia Suluhu hivyo ni vyema wakajisajili mapema wapate fursa hiyo.

Aidha, Lyaniva ameliagiza Shirika la Viwanda Vidogo (SIDO) na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kuandaa programu ya mafunzo kwa wanawake ambayo itakuwa na tija ya kuwaelimisha na baadae wataweza kujiajiri, hivyo programu hiyo iwasilishwe kwa Mkuu wa Mkoa ndani ya mwezi mmoja.

Akizungumza Mkurugenzi wa IBRA Contractors na Rais wa Sauti ya Wanawake Wajasiriamali Tanzania (VoWET), Maida Waziri amewataka wanawake nchini kujituma na kuwa wabunifu katika biashara zao jambo litakalo wapelekea kufanikiwa, huku akisisitiza elimu na mtaji siyo chanzo cha kukata tamaa bali kufanya kazi kwa bidii na kutumia taarifa sahihi zitakazo wapelekea kufanukiwa kama ilivyokuwa kwake, ambaye amefikia hatua ya kupewa tuzo na Rais Mstaafu Jakaya Kikwetu kwa kuwa Mkandarasi bora 2011-2015.

Siku ya Wanawake Duniani husherekewa Machi 8 kila mwaka, ambapo kitaifa imesherekewa Mkoani Singida na mgeni Rasmi alikuwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu, huku kauli mbiu ikiwa Tanzania ya Viwanda Mwanamke ni Msingi wa Mabadiliko ya Kiuchumi.

Serikali yaahidi kuvilinda vyombo vya habari vilivyowekeza nchini
Mwenyekiti, Katibu Chadema Lindi watoka Gerezani